Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa
familia za watu 29 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani
iliyosababishwa na mabasi mawili ya kampuni moja ya City Boy kugongana uso kwa
uso katika kijiji cha Maweni, kilichopo katika tarafa ya Kintinku, Wilaya ya
Manyoni Mkoani Singida.
Ajali hiyo
imetokea leo tarehe 04 Julai, 2016 majira ya saa tisa alasiri wakati basi moja
la kampuni ya City Boy lenye namba T531DCE lililokuwa likisafiri kutoka Jijini Dar
es salaam kwenda Kahama Mkoani Shinyanga lilipokuwa likipishana na basi jingine
la kampuni hiyo hiyo ya City Boy lenye namba T247DCD lililokuwa likisafiri
kutoka Kahama Mkoani Shinyanga kwenda Jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli
ametuma salamu zake kwa familia zilizopatwa na msiba huo kupitia kwa Mkuu wa
Mkoa wa Singida Mhandisi Methew Mtigumwe na kuelezea masikitizo yake juu ya
kutokea kwa ajali hiyo mbaya, iliyosababisha watu wengi kufariki dunia.
"Nimepokea
kwa mshituko mkubwa taarifa za ajali hii ambayo imesababisha vifo vya idadi
kubwa ya watanzania, kwa hakika nimesikitishwa sana sana na napenda kuungana na
familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu katika kipindi hiki kigumu cha
majonzi.
"Namuomba
Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu wanafamilia wote waliopoteza
jamaa zao, na sote tuwaombee marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi,
amina." Ameeleza Rais Magufuli.
Aidha, Dkt.
Magufuli amewaombea majeruhi wote wa ajali hiyo, ambao wanapatiwa matibabu
hospitali wapate nafuu na kisha kupona haraka ili warejee majumbani kwao
kuungana na familia zao katika shughuli za kila siku.
0 comments:
Post a Comment