Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake ya awamu ya
tano itahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapatiwa mikopo, lakini haitakubali
kulekeza mikopo hiyo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu.
Rais Magufuli
ametoa kauli hiyo leo tarehe 02 Juni, 2016 wakati akizungumza na Jumuiya ya
Chuo Kikuu cha Dar es salaam muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la
ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho inayojengwa katika kampasi ya Mlimani
upande wa mashariki mwa chuo.
Akiwahutubia
maelfu ya wanajumuiya hiyo wanaojumuisha wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wa
chuo, Dkt. Magufuli amesema serikali yake imedharia kutoa elimu bora kwa
watanzania na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto mbalimbali
zinazovikabili vyuo, lakini ameelezea kusikitishwa kwake na uwepo wa wanafunzi
waliodahiliwa na baadhi ya vyuo hapa nchini pasipo kuwa na sifa zinazomwezesha
mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu.
"Wapo
wanaokopeshwa mikopo hii ya elimu ya juu lakini hawana sifa, Mheshimiwa Profesa
Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Ufundi) nakushukuru kwa hatua unazozichukua katika
kusafisha wizara yako na hili nalisema kwa uwazi, na ukweli lazima usemwe hata
kama ni mbele ya wanachuo.
"Una D,D
unasajiliwa kuchukua digrii chuo kikuu na unapata mkopo wa serikali, ni aibu ya
ajabu, haiwezekani, haiwezekani, haiwezekani. Lakini wakati tunawalipia
wanafunzi 489 waliomaliza kidato cha nne na kupata D,D manaake wengine ni
divisheni 4, kuchukua digrii, wapo wanafunzi wengine wa kidato cha sita
wamekosa mikopo, wapo wanafunzi wengine walio na diploma wamekosa mikopo" Amesema
Rais Magufuli.
Rais Dkt. John
Pombe Magufuli pia amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa nchini kuacha
kujihusisha na masuala ya siasa na badala yake wazingatie jukumu kuu
lililowapeleka vyuoni ambalo ni kusoma, huku akibainisha kuwa serikali yake
haitavumilia vitendo vya vurugu vyuoni.
"Ifike mahali
watanzania tukubali ukweli, tuache siasa kwenye masuala ya msingi, ukimpeleka
mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye ufaulu wa divisheni 4, anachukua digrii,
akishatoka pale, hata kama atafanikiwa kupata digrii itakuwa ni ajabu.
"Lakini
niwaombe wanafunzi mahali kote, msitumiwe na wanasiasa, mmekuja kusoma, someni,
siasa mtazikuta mkiondoka, nawambia mmekuja kusoma someni, na ndio maana hata
katika kutoa mikopo hatubagui, sijui huyu CCM, sijui huyu CHADEMA, sijui huyu
nini, nyie wote ni watanzania, ndio lengo letu. Amesisitiza
Dkt. Magufuli.
Amewaahidi kuwa
serikali yake itahakikisha inatoa mahitaji ya wanafunzi ikiwemo mikopo na
kuboresha miundombinu ya vyuo, lakini amewataka wanavyuo nao kuwa wavumilivu na
wazalendo pale ambapo mahitaji hayo yatachelewa kutokana na mchakato wa
kuyapata kuhitaji muda.
Kabla ya
kuwahutubia wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mkuu wa chuo hicho
ambaye ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemuomba
Rais Magufuli asaidie kuboresha miundombinu ya chuo hicho ikiwemo ujenzi wa
mabweni ya wanafunzi ambao kwa takribani asilimia 70 wanaishi nje ya chuo,
ambapo Rais Magufuli ameahidi kutoa shilingi bilioni 10 na ameuagiza uongozi wa
chuo hicho kuainisha eneo ndani ya chuo ili ujenzi wa mabweni uanze mara moja.
Uzinduzi wa ujenzi
wa Maktaba hiyo ya kisasa umehudhuriwa na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu
Youqing ambaye nchi yake ndio imetoa msaada wa dola za Marekani zaidi ya
Milioni 41 kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba hiyo.
Maktaba hiyo ya
kisasa itakapokamilika itakuwa ndio maktaba bora kuliko zote barani Afrika,
ikiwa na ukubwa wa eneo la meta za mraba 20,000 na itakuwa na uwezo
wa kuwa na vitabu 800,000 na kuchukua wanafunzi 2,600 kwa mpigo.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
02 Juni,
2016
0 comments:
Post a Comment