![]() |
Kanisa la Waadventista wa Sabato kupitia shirika la
maendeleo na misaada ADRA Tanzania, limetoa msaada wa thamani ya Tsh.
46M kwa Mkoa wa Kagera, kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea hivi
karibuni mkoani hapa.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa niaba
ya Kanisa, kaimu mkurugenzi wa ADRA Tanzania ndugu Elamu Bunde, amesema
Kanisa limeguswa sana na tatizo walilopata wananchi wa Kagera na
kuongeza kuwa Kanisa litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ili
kuhakikisha maisha ya wahanga wa tetemeko yanarudi katika hali ya
kawaida.
Akipokea msaada huo mkuu wa Mkoa wa Kagera meja jenerali
mstaafu SALUMU MUSTAFA KIJUU, amelishukuru kanisa la Waadventista wa
Sabato kwa kuwa mstari wa mbele kwakutoa na kuongeza kuwa hiyo ndiyo
dini ya kweli. Kijuu ameongeza kuwa Mkoa wa Kagera bado unahitaji msaada
mkubwa kutokana na athari kubwa zilizojitokeza katika miundombinu ya
huduma za kijamii kama barabara, shule na hospitali.
Aidha mkuu wa Mkoa amezitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni
pamoja na vifo vya watu 17, majeruhi 440 kati ya hao 23 wamefanyiwa
upasuaji mbalimbali kutokana na kuvunjika baadhi ya sehemu za miili yao.
Katika tetemeko hilo jumla ya majengo 2072 yalianguka kabisa, 16595
yamepata mipasuko hatarishi na hayafai kukaliwa na watu na jumla ya
nyumba 9927 zimepata mipasuko inayoweza kutengenezwa.
Hata hivyo KIJUU hakutaka kufafanua juu ya kiasi gani cha
fedha kiliingizwa kwenye akaunti bandia ya maafa iliyofunguliwa kinyume
na utaratibu wa serikali na baadhi ya watumishi wa mkoa kwa madai kuwa
jambo hilo liko mahakamani. KIJUU ameongeza kuwa wananchi walioathirika
wanapaswa kuanza kukarabati nyumba zao kwakuwa serikali itaanza
kukarabati miundombinu ya huduma za jamii kama barabara, shule na
hospitali.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa mkoa, tadhimini
iliyokwisha kufanyika, zinahitajika Tsh 10 billion kurejesha miundo
mbinu ya huduma za kijamii katika hali yake ya kawaida na 880 bilion
kujenga nyumba 16,595 zilizo athirika mkoani hapa.
0 comments:
Post a Comment