![]() |
![]() |
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali imeamua
kusimamisha kwa muda mfupi usiozidi miezi miwili zoezi la utoaji ajira mpya na
upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma kwa lengo la kupisha uhakiki wa
watumishi wa umma katika orodha ya malipo ya mshahara na kuondoa watumishi
hewa.
Rais Magufuli
amesema hayo leo tarehe 22 Juni, 2016 katika Jubilei ya miaka 50 ya Benki Kuu
ya Tanzania (BOT) iliyofanyika katika ukumbi wa Benki hiyo, Mtaa wa Mirambo
Jijini Dar es salaam.
Dkt. Magufuli
amesema zoezi hilo halina nia ya kuwakatisha tamaa watumishi wa umma na
amewahakikishia watumishi wote wa umma kuwa serikali itaendelea kuajiri
watumishi wapya na kuwapandisha vyeo waliopo kama kawaida mara baada ya
kukamilika kwa zoezi.
"Serikali
ninayoiongoza haina nia ya kuwakatisha tamaa wafanyakazi, lengo lake ni
kujipanga kwa makosa tuliyoyafanya, na ndio maana nimesema kwa kipindi cha
mwezi mmoja hivi au hata mwezi mmoja na nusu, haitazidi miezi miwili, tusiajiri
mtumishi yeyote serikalini, lakini pia katika kipindi cha mwezi mmoja
hatutawapandisha vyeo wafanyakazi, ninaomba wafanyakazi waelewe hili, kwa
sababu tukiendelea tutakuwa tunawapandisha vyeo hata wafanyakazi ambao hawapo,
tunafanya ukaguzi wote tukishamaliza wafanyakazi wataendelea kupandishwa
vyeo" amesema Rais Magufuli.
Wakati
huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameipongeza
Benki Kuu ya Tanzania kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kipindi cha miaka 50
katika kusimamia sekta ya fedha na maendeleo, lakini ameitaka benki hiyo
kuchukua hatua za haraka dhidi ya baadhi ya changamoto zinazoyahusu majukumu
yake.
Miongoni mwa
changamoto hizo ni idadi ndogo ya watanzania wanaonufaika na huduma za benki
hususani waishio vijijini, benki kutoza riba kubwa na hivyo kusababisha
wananchi kuogopa kukopa kwa hofu ya kushindwa kulipa, kuilinda thamani ya
Shilingi ya Tanzania, na kukusanya kodi ipasavyo kwa miamala inayofanywa
kupitia simu za mkononi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano
Tanzania (TCRA).
Changamoto
nyingine ni kusimamia ipasavyo maduka ya kubadilishia fedha (Bureau de change) ili kuthibiti utakatishaji na
utoroshaji wa fedha na kuhakikisha ushukaji wa mfumuko wa bei uliotoka asilimia
28 hadi kufikia asilimia 5.1 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita unaonesha
matokeo katika nafuu ya maisha ya watanzania.
Aidha, Rais
Magufuli ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuchukua hatua mara moja dhidi ya
benki ambazo hazizalishi faida zikiwemo benki za serikali, kufuta account mfu
(Domant account) na kuanzisha mara moja akaunti moja ya mapato na matumizi ya
serikali (Single Treasury Account)
Jubilei hiyo
imehudhuriwa na Magavana na Manaibu Gavana kutoka nchi 18 za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), Mabalozi
kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa Taasisi za fedha za Afrika na Makatibu
wakuu wa Wizara za Fedha na Mipango wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
22 Juni,
2016
0 comments:
Post a Comment