Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumamosi
tarehe 07 Mei, 2016 amewatunuku Kamisheni Maafisa wapya 586 wa Jeshi la Ulinzi
la Wananchi Tanzania (JWTZ) kundi la 58/15 waliomaliza mafunzo yao katika Chuo
cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli (TMA) Mkoani Arusha.
Maafisa hao wapya
wa Jeshi walianza kozi yao tarehe 04 Mei, 2015 na wamepewa cheo cha Luteni usu.
Kati ya maafisa
wapya waliohitimu kozi yao leo, 80 ni madaktari na 6 ni marubani wa ndege
waliopata mafunzo yao katika nchi tatu ambazo ni Tanzania, Uganda na Afrika
Kusini.
Kabla ya kutunuku
Kamisheni kwa maafisa hao, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekagua gwaride la
maafisa hao wapya na pia amepokea heshima ya gwaride lililopita mbele yake kwa
mwendo wa pole na haraka, na baadaye kusikiliza ujumbe juu ya utendaji kazi wa
serikali ya awamu ya tano, nidhamu ya kazi na uzalendo kupitia muziki wa bendi
na kwaya.
Katika hatua
nyingine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa
mara nyingine amelazimika kuzungumza na wananchi wa Arusha Mjini waliokuwa
wamezuia msafara wake uliokuwa ukitoka Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli
kwenda Ikulu ndogo ya Arusha, na kuwahakikishia kuwa serikali yake imeanza
kuwashughulikia wafanyabiashara ambao wameficha sukari kwa makusudi na
kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo.
Rais Magufuli
amesema tayari vyombo vya dola vimekamata tani 5,000 za sukari iliyofichwa na mfanyabiashara
mmoja huko Tabata Jijini Dar es salaam na pia vimembaini mfanyabiashara
mwingine aliyeficha sukari hiyo Jijini Arusha.
"Kweli
nitawakomesha hawa, wasije wakanilaumu, haiwezekani ukaficha sukari wakati
viwanda vyetu vinatengeneza sukari, kuna mmoja mwingine yupo Arusha hapa, nae
ameficha sukari, alienda akanunua kwenye viwanda vya sukari vya hapa akaificha
yote, leo ninamshughulikia.
"Kuna
mwingine alinunua sukari pale Kilombero zaidi ya tani 3,000 akaficha, na
mwingine ameshikwa pale Tabata alikuwa ameficha tani 5,000, na wanasubiri
katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili ndugu zetu Waislamu wapate shida, haya ni
mashetani makubwa, unawafichia watu chakula ambacho wanatakiwa kula, lakini
nataka niwahakikishie ndugu zangu, hili ni tatizo la muda Tanzania, sukari itapatikana
kwa wingi, na itanunuliwa na serikali, tumeshaagiza sukari lakini hatutawapa
vibali hawa wafanyabiashara ambao wanatunyonya, tutanunua wenyewe na tutauza
bei ya chini, hilo ndio lengo la serikali"
Amesema Rais Magufuli
Aidha, Rais
Magufuli amerejea kauli yake kuwa serikali yake haitawavumilia viongozi na
watumishi wa umma ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na
ufisadi, huku akisema ataendelea kutumbua majipu kwa yeyote atakayebainika
kuchezea mali za umma ili kulinda maslai ya wengi, hususani watanzania
wanyonge.
"Ninafanya
kwa niaba yenu, ninafanya kwa niaba yenu, ningekuwa sifanyi kwa niaba yenu, na
mimi ningeingia madarakani ningeanza kushirikiana na hao, na wengine
walifikiria nitashirikiana nao, wamekwama mimi nitawatumbua kila siku ili
Tanzania iwe ya neema iweze kwenda mbele, haiwezekani nchi kama hii tajiri,
Tanzanite ipo, dhahabu ipo, wanyama mpaka nyani wameanza kuuzwa, wakimalizika
nyani si tutauzwa na sisi ndugu zangu, ni lazima nisimamie hili"
amesisitiza Dkt. Magufuli.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
07 Mei,
2016
0 comments:
Post a Comment