![]() |
Picha
namba 2-3. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na mgeni wake Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake
nchini Francisco Montecillo.
|
![]() |
Picha
namba 4. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiagana na Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake Francisco
Montecillo Ikulu jijini Dar es Salaam.
|
![]() |
Picha
namba 4. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiagana na Balozi wa Vatican hapa nchini anayemaliza muda wake Francisco
Montecillo Ikulu jijini Dar es Salaam.
|
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameikaribisha nchi ya Canada
kushirikiana na serikali yake ya awamu ya tano katika kuleta mageuzi ya
kiuchumi, hususani katika uwekezaji kwenye sekta ya Kilimo, Madini, Uvuvi na Huduma
za kijamii.
Rais Magufuli
ametoa ujumbe huo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Canada hapa nchini
Mheshimiwa Alexandre Le've'que aliyekutana nae Ikulu Jijini Dar es salaam na
kupokea barua yenye ujumbe wa Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa Justin Trudeau.
Katika mazungumzo
hayo, Rais Magufuli amesema serikali yake hairidhishwi na jinsi kilimo cha Tanzania
kisivyowanufaisha wakulima ipasavyo, na hivyo ameikaribisha nchi ya Canada
hususani sekta binafsi ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kujenga viwanda
vya kusindika mazao ya kilimo na uvuvi ili kuzalisha ajira na kuongeza thamani
ya mazao kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
Dkt. Magufuli pia
ametaka Canada yenye uwezo mkubwa kiteknolojia na mtaji ishirikiane na Tanzania
katika uwekezaji kwenye sekta ya madini na gesi kwa kujenga viwanda vya
kuchakata madini ndani ya nchi ya Tanzania na pia rasilimali ya gesi ambayo
mpaka sasa Tanzania imethibitika kuwa na hifadhi ya futi za ujazo zaidi ya
Trilioni 57.
"Mheshimiwa
Balozi Alexandre Le've'que naomba ukamweleze Waziri Mkuu wa Canada Mheshimiwa
Justin Trudeau kuwa Tanzania na Canada sio tu ni nchi marafiki bali pia ni
ndugu wenye uhusiano wa kihistoria. Ningependa kuona Canada inashirikiana na
serikali yangu, katika juhudi zake za kuachana na usafirishaji wa mchanga wa
madini badala ya madini yaliyochakatwa na pia kuachana na usafirishaji wa mazao
yakiwa ghafi" Amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake
Balozi wa Canada hapa nchini Mheshimiwa Alexandre Le've'que amemhakikishia Rais
Magufuli kuwa atafikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu Canada Mheshimiwa Justin
Trudeau, na amebainisha kuwa nchi hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania
katika juhudi zake za kuimarisha uchumi, hasa baada ya kujionea juhudi za Rais
Magufuli katika kukabiliana na rushwa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na
kusimamia nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais
wa Aljeria Mheshimiwa Abdelaziz Bouteflika ambaye pamoja na kumpongeza kwa
hatua anazochukua katika uendeshaji wa serikali, amemhakikishia kuwa Aljeria
ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania
huku akitaja maeneo ya kipaumbele kuwa ni nishati na kilimo.
Ujumbe wa Rais
Bouteflika umewasilishwa kwa Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam na Balozi
wa Aljeria hapa nchini Mheshimiwa Belabed Saada.
Rais Magufuli
amemhakikishia Rais Bouteflika kuwa Serikali yake itaendeleza na kuimarisha
uhusiano na ushirikiano na Aljeria, na kwamba hivi karibuni imepanga kuanzisha
ofisi za Ubalozi katika nchi hiyo.
Kuhusu sekta za
nishati na kilimo, Rais Magufuli amesema serikali yake inakaribisha uwekezaji
kutoka Aljeria hasa wakati huu ambapo Tanzania imethibitika kuwa na kiasi
kikubwa cha gesi, na kwa upande wa kilimo ametoa wito kwa Aljeria kushirikiana
na Tanzania katika mpango wake wa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao,
ikiwemo usindikaji wa zabibu, viwanda vya nguo, viwanda vya ngozi na nyama na
viwanda vya kusindika minofu ya samaki.
"Naomba
ukamweleze Mheshimiwa Rais Bouteflika kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha
zaidi ushirikiano wake na Aljeria na kwamba imefurahishwa sana kuona Aljeria
ipo tayari kusaidia juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo nchini Tanzania" Rais Magufuli amemweleza Balozi Belabed Saada.
Katika
hatua nyingine, Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ameagana na Balozi wa Vatican hapa nchini Mheshimiwa Francisco Montecillo
ambaye anamaliza muda wake baada ya kuiwakilisha Vatican kwa muda wa miaka
minne na nusu.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es
salaam
22 Aprili,
2016
0 comments:
Post a Comment